News

Vijana Wilayani Hai Kukopeshwa Bajaji Wajiajiri

Vijana Wilayani Hai Kukopeshwa Bajaji Wajiajiri

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya ameahidi kutoa mkopo wa Bajaji 15 kwa vijana madereva wa bajaji wa wilaya hiyo ili kuwawezesha vijana hao kujiajiri na kuchangia pato la Taifa.

Ole Sabaya amesema hayo wakati akizungumza na madereva bajaji wa Hai mjini katika kikao kilicholenga kufanya tathmini ya utatuzi wa changamoto zinazowakumba madereva hao zilizowasilishwa kwenye kikao cha awali kilichofanyika mwezi Mei mwaka huu kikiwakutanisha madaereva bajaji na mkuu huyo wa wilaya.

Ole Sabaya amemtaka mwenyekiti wa madereva Bajaji Pendaeli Nkya kuweka utaratibu wa wazi wa kupata majina ya madereva wanaohitaji mikopo ndani ya vikundi vyao ili wapatiwe Mikopo hiyo na kuondoa changamoto zinazowakumba katika kazi hiyo.

Amesema kuwa baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na madereva hao ni pamoja na ubovu wa baadhi ya barabara ikiwemo ya St. Dorkas iliyopo katika kata ya Muungano ndani ya mamlaka ya mji mdogo wa Bomang’ombe ambayo hivi sasa imeshaanza kufanyiwa ukarabati kwa kiwango cha changarawe.

Aidha amesema pamoja na kutatua kero hizo serikali itaendelea kuwa nao wakati wote na kwa changamoto zozote kwani madereva bajaji wanafanya kazi vizuri na kuwataka waendelee na uaminifu katika kazi yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Hai (DTO) Mbarouk Abdalah amesema kuwa hali ya usalama barabarani kwa wilaya ya hiyo iko salama na kuwataka madereva kuendelea kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuacha tabia ya kuzidisha abiria kwenye vyombo vyao jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.

Na baadhi ya madereva wameishukuru serikali ya wilayani Hai kwa kusikiliza kero zao na kuzitatua kwa wakati huku wakimpongeza mkuu wa wilaya hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea wanyonge.

Mkuu wa Wilaya ya Hai mara ya mwisho alifanya mkutano na madereva hao ambapo alipokea kero mbalimbali zinazowakabili kwenye majukumu yao na kuendelea kutatua baadhi ya kero ikiwemo ubovu wa barabara unaosababisha kuharibu vyombo vyao ambazo hadi kufanyika kwa kikao cha pili barabara zote za maeneo ya Mji Mdogo wa Hai zimerekebishwa na nyingine zikiendelea kushughulikiwa.

Demo

Related Articles

Leave a Reply

Close