News

Mwenyekiti ZEC Aridhishwa Uboreshaji Daftari Wapiga Kura Wilaya ya Hai

Mwenyekiti ZEC Aridhishwa Uboreshaji Daftari Wapiga Kura Wilaya ya Hai

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Mhe. Hamad Mahmood ameridhishwa na huduma zinazotolewa kwa wananchi kwenye vituo vya kuandikishwa wapiga kura katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Ametoa kauli hiyo mapema leo tarehe 21/7/2019 alipofanya ziara ya kikazi kuangalia maendeleo ya zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaloendelea kwenye mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Akiwa wilayani Hai ametembelea vituo mbalimbali vinavyoshughulikia maboresho ya daftari hilo na kupokea taarifa za utekelezaji wa kazi kwenye kituo husika ikiwa ni pamoja na kusikiliza changamoto zinazojitokeza kwenye zoezi hilo.

Akiwa kwenye ziara hiyo Mahmood ametembelea vituo mbalimbali vinakofanyika zoezi hilo ikiwemo vituo vya Kata ya Machame Kaskazini ambapo amefurahishwa kuona namna zoezi linavyoendeshwa kwa uwazi hasa baada ya kukutana na mawakala wa vyama tofauti vya siasa wakifuatiliza utekelezaji wa zoezi hilo.

Aidha amewataka watendaji wanaoshiriki zoezi hilo kutekeleza kwa uaminifu majukumu waliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kufanikisha zoezi.

Pamoja na hayo Mahmood amewakumbusha watendaji hao kutumia kwa uangalifu vifaa vinavyotumika kwa zoezi hilo kwani vimepatikana kwa fedha nyingi lakini pia amewataka kuvitunza ili vikatumike kwenye zoezi kama hilo kwenye mikoa na Halmashauri nyingine.

Zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linafanyika kwa pamoja kwenye mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambapo lilianza tarehe 18/07/2019 na linatajiwa kukamilika tarehe 24/07/2019 na wanaohusika na zoezi hilo ni wale ambao hawana kadi ya kupigia kura, wale waliopoteza na wale ambao kadi zao za kupigia kura zimeharibika.

Demo

Related Articles

Leave a Reply

Close